
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi kujenga tabia ya kujiwekea akiba ya fedha kwenye taasisi za kifedha kwa kuwa ni nguzo muhimu kwa maendeleo yao. Aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akizindua Mpango wa Pili wa Taifa Huduma Jumuishi za Fedha wa Mwaka 2018 hadi 2022.
Alisema katika Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Huduma Jumuishi wa mwaka 2014-2016, mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa asilimia 86 mwaka 2017, kutoka asilimia 29 mwaka 2012 ya wananchi walio karibu na huduma za kifedha.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za kifedha nchini imefikia asilimia 65 na kuifanya Tanzania kuwa ya kwanza barani Afrika na ya sita duniani kwa kuboresha mazingira ya upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi.
Ili kuhakikisha Mpango huo wa Pili wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha unafanikiwa katika kuwafanya wananchi kujenga tabia ya kujiwekea akiba ya fedha, Waziri Mkuu alisema, “Tunataka kuongeza kiwango cha wananchi wanaojiwekea akiba ya fedha kupitia mifumo rasmi kutoka asilimia 43 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 60 mwaka 2022.
“Kuongeza kiwango cha wananchi kuwa karibu na huduma za kifedha katika umbali usiozidi kilomita tano kutoka asilimia 86 ya mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 90 mwaka 2022; kuongeza kiwango cha wananchi wanaotumia mara kwa mara huduma za kifedha kupitia asasi za fedha na mitandao ya simu kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 75 mwaka 2022.”
Malengo mengine ya Mpango huo wa Pili kwa mujibu wa Waziri Mkuu ni kuongeza kiwango cha wananchi wanaotumia huduma za bima kutoka asilimia 45 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 50 mwaka 2022, kuongeza kasi ya kuwawezesha wananchi kuwa na vitambulisho vya taifa kutoka asilimia 23 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 90 mwaka 2022.
Aidha, alisema kuwa kupitia mpango huo, serikali inataka kuongeza matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika kutoa huduma za kifedha nchini. Alisema mpango huo wa Huduma za Kifedha ni muhimu kwa kuwa utalisaidia Taifa katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, kukuza uchumi wa wananchi na kupunguza umaskini. Kutokana na umuhimu wa mpango huo, Waziri Mkuu alisema serikali inasisitiza kuendelea kuwepo kwa ushirikiano imara kati ya sekta binafsi na sekta ya umma.
Alisema serikali itaendelea kuimarisha miundombinu kama vile ya umeme, kuweka mazingira wezeshi ya huduma za kifedha ili kuondoa vikwazo kwa watoaji na watumiaji wa huduma za kifedha nchini. Kwa upande mwingine, serikali imewataka wajumbe wa Baraza la Taifa la Mpango Huduma Jumuishi za Kifedha kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali kama vile vyombo vya habari na makongamano ili wananchi wengi wajue umuhimu wa huduma za kifedha kwenye maisha yao.
No comments:
Post a Comment