Spika EALA aahirisha bunge kupisha maridhiano


SPIKA wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Martin Ngoga amelazimika kusitisha shughuli za Bunge hilo hadi hapo zitakapoitishwa tena baada ya wabunge wa Tanzania na Burundi kutangaza kutomtambua.
Ngoga alitangaza kusitishwa kwa shughuli za Bunge hilo jana na kusema hawezi kuruhusu likaendelea kwa hatua za kuchagua wajumbe wa kamati zake, huku nchi nne tu za Sudan Kusini, Rwanda, Kenya na Uganda zikishiriki na nchi nyingine mbili zikisusa.
"Siwezi kuendelea na bunge hili kwa sababu ya akidi kutotimia, maana hatutaweza kuchagua kamati mbalimbali kutokana na mzozo wa kutonitambua mimi kama Spika. Naahirisha Bunge hili hadi hapo mtakapotangaziwa rasmi,” alisema. Hata hivyo, wakati Spika huyo alipolazimika kuahirisha Bunge hilo, tayari wabunge walikuwa wamefanya kazi ya kuchagua Kamati ya Uongozi na ndipo baadaye Bunge likaahirishwa.
Juzi wabunge wa EALA kutoka Tanzania na Burundi, walitangaza rasmi kutomtambua na kushirikiana na Spika Ngoga kutoka Rwanda, aliyechaguliwa juzi na wabunge kutoka nchi nne, badala ya sita zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Tanzania, Dk Ngwaru Maghembe alisema wabunge wa mataifa hayo manne, waliendesha uchaguzi bila kuhusisha wenzao wa nchi mbili za Tanzania na Burundi wakati wanajua wanakiuka Kanuni na Sheria za Mkataba wa EAC.
Alisema wabunge wote wa Bunge hilo walipofika Arusha, walipewa fomu za kuomba kuwania nafasi ya Uspika katika Bunge hilo na ndio maana wabunge kutoka nchi tatu, ambao ni Adam Kimbisa kutoka Tanzania, Ngoga kutoka Rwanda na Leontine Nzeyimana kutoka Burundi, walichukua fomu kuwania nafasi hiyo kwa vile Kanuni zinaruhusu.
"Sheria ya Mkataba wa EAC Kifungu cha Namba 6 (c) inafafanua kuwa watafanya uchaguzi kwa maridhiano na si kufuata silabi za nchi, bali kila mtu ana haki ya kugombea nafasi hiyo kwa kila nchi," alisema.
Mbunge Dk Abdullah Makame wa Tanzania alisema Katibu wa Bunge hilo, Kenneth Maddete amekiuka Mkataba wa EAC na Kanuni za EALA na zinazotamka kuwa kutakuwa na hoja ya kupiga kura ili kumchagua Spika. “Ndiyo maana Katibu wa Bunge la EALA, Maddete alieleza kuwa wagombea watatu walikuwa wamechukua fomu kuwania nafasi hiyo ya uspika, kwa vile anajua Kanuni na sheria zilikuwa zinawapa haki ya kupigiwa kura.
"Tunahitaji jumuiya ya utashi wa kisiasa na moyo wa kuvumiliana, ndio maana tuliwasubiri wenzetu wa Kenya tukachelewa kuanza Bunge.” Alisisitiza kuwa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, pia ipo na itatumika katika kutoa ufafanuzi juu ya jambo hilo la uchaguzi wa Spika. Mwenyekiti wa wabunge kutoka Burundi, Victor Burikukiye alisema hawamtambui Spika huyo kutoka Rwanda.
Alisema watu wanaweza kutafsiri vile wanavyojua, lakini Katibu Mkuu wa EALA alitoa barua kwa wabunge watatu kuwania nafasi hiyo kwa kujua kuwa wanayo haki. "Huu ni uchaguzi gani wa nchi nne kufanya uchaguzi na tunasema hatutambui uchaguzi wa Spika uliofanyika bila ya kuwepo kwa wabunge wa Burundi," alisema.
Spika anachaguliwa kwa mzunguko na sasa hivi uspika ulikuwa ni zamu ya Burundi, Rwanda na Sudan Kusini na hii nafasi hii ilikuwa ni yetu ya Burundi, kwanini watufanyie hivi,” alisema. Mbunge kutoka Uganda, Chris Opoke alisema wabunge hao wamepoteza miezi sita bila kuanza kwa bunge, hivyo hawaoni sababu ya kuchelewa tena kuendelea na bunge hilo kwa sababu ya kukosekana kwa spika, hivyo aliunga mkono Spika huyo kuchaguliwa.
Share:

No comments:

Popular Posts

Followers

Search This Blog

My Blog List

Labels

Contributors

Recent Posts

Pages