Sikujua tumbaku ingegeuka janga kwangu
ALIPOANZA kusokota tumbaku na kuvuta akiwa na umri wa miaka 24, Maine Mshomi aliichukulia kuwa ni kiburudisho. Hakuota abadani kwamba ‘kiburudisho’ hicho kingegeuka janga katika maisha yake.
Akiwa sasa na umri wa miaka 55, Mshomi ambaye ni mkazi wa kijiji cha Lugine wilayani Kiteto katika Mkoa wa Manyara, anakumbuka alivyokuwa akivuta misokoto ya tumbaku kati ya minne na mitano kwa siku. Tumbaku aliyokuwa akivuta alikuwa akiipata kijijini ambako inalimwa lakini si kwa ajili ya biashara bali kwa matumizi yao.
Anasema alipokuwa akienda katika maeneo yenye mkusanyiko wa watu, alikuwa akivuta sigara. Wakati mwingine alipatwa na mawazo ya kuacha kutumia tumbaku hususani alipokuwa hana fedha, lakini alipopata fedha aliendelea kuvuta.
Mshomi mwenye watoto wanne, anasimulia haya yote akiwa kitandani katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road, jijini Dar es Salaam. Amepimwa na kubainika kwamba anasumbuliwa na saratani ya koo.
Kabla ya kufika hospitalini hapo, alishakwenda hospitali nyingine kutafuta tiba bila mafanikio. Hospitali hizo ni Mvumi iliyopo mkoani Dodoma pamoja na KCMC ya mkoani Kilimanjaro.
Anasema amekuwa akijigharimia matibabu na sasa ameshatumia si chini ya Sh milioni 1.7. Samueli Mshomi ni ndugu yake wa karibu anayesimulia kuwa kaka yake alianza kuugua Machi mwaka huu na Ocean Road walifika Agosti mwaka huu.
“Kaka yangu amevuta tumbaku kwa muda mrefu sana, takribani kipindi cha chote ujana wake,” anasema Samueli. Anaongeza: “Tulimshauri kuacha alipoanza kuumwa japokuwa yeye mwenyewe hakuwa tayari kwa madai kwamba daktari hajamwambia kama ugonjwa wake umechangiwa na matumizi ya tumbaku.”
Hata hivyo, anasema maelezo ya daktari yalionesha moja kwa moja kuwa matumizi ya tumbaku yamechangia kwa kiasi kikubwa katika ugonjwa wa ndugu yao. Samuel anasema mpaka sasa kaka yake haamini kama tatizo lake limesababishwa na matumizi ya tumbaku akihoji kwamba mbona kuna wagonjwa wengine wanaugua saratani na hawajawahi kutumia tumbaku?
Samueli anasema ipo haja ya serikali kutoa elimu ya kutosha hasa kwa wakazi wa vijijini kuhusu madhara makubwa yanayoletwa na utumiaji wa tumbaku. Mkazi huyo wa kijiji cha Songambele anasema matumizi ya tumbaku yako juu sana kijijini kwao.
Anatamani ingewezekana, serikali izuie uzalishaji wa tumbaku kutokana na madhara yake kiafya. Wakati wa maadhimisho ya siku ya kupinga matumizi ya tumbaku Mei mwaka jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema tafiti zinaonesha takribani watu milioni sita hupoteza maisha duniani kwmwaka kutokana na utumiaji wa tumbaku na bidhaa zake.
Akielezea uhusiano wa tumbaku na saratani, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga ya Saratani katika Hospitali ya Taifa ya Ocean Road, Dk Chrispin Kahesa anasema tumbaku ina kemikali zaidi ya 200 na kati ya hizo 69 zinahusishwa na saratani.
“Saratani kwa ujumla ni mkusanyiko wa magonjwa zaidi ya 200, inategemea tu ni saratani ya eneo gani, mfano, titi, koo, shingo ya uzazi na kadhalika,” anasema. Anasema takribani saratani zote zinahusishwa na tumbaku lakini zaidi ni saratani zinazoathiri maeneo ya mfumo wa chakula.
Akifafanua kitaalamu, anasema mfumo wa chakula unaanzia kwenye kinywa ukihusisha ulimi, mdomo, njia za hewa koo na tumbo. “Kuna saratani nyingine zaidi zinaongezeka kama vile saratani za kibofu, mapafu, shingo ya kizazi na kadhalika kwa sababu hizi kemikali ukizivuta zinaingia kwenye nji ya hewa lakini zinasambaa kwenye damu hadi zinakwenda kuathiri maeneo mengine,” anasema.
Anaongeza: “Kwa hiyo tafiti zinaonesha zile saratani ambazo zinaanzia kwenye njia ya chakula na mfumo wa hewa unaohusisha pia mapafu ndizo huwaathiri wengi zaidi. Anasema athari za tumbaku siyo kwa wanaotumia kwa kuvuta pekee bali hata wanaomung’unya kama wala ugoro huathirika eneo la kinywa au njia ya chakula. Dk Kahesa anasema saratani za njia ya kinywa na chakula zinaongezeka nchini.
Anasema kwa wanaume saratani inayoongoza ni ya ngozi ikifuatiwa na ya njia ya chakula ambayo kwa kiwango kikubwa inachangiwa na matumizi ya tumbaku. Hata hivyo, anasema idadi ya wagonjwa inayoonekana hospitalini ni ndogo kwa maana upo uwezekano wa wengine kufariki bila kutambulika kutokana na kutopata fursa ya kufika katika maeneo ya tiba.
“Kwa mfano, ukienda Katavi kuna matatizo mengine ya kiafya ambayo yanaendana kabisa na matumizi ya tumbaku kama vile upungufu wa nguvu za kiume,” anasema. Anasema wengine wanaotumia tumbaku pia ni watumiaji wazuri wa vitu vingine hatarishi ikiwemo pombe.
“Tumbaku inaweza kuhamasisha matumizi ya vitu vingine lakini yenyewe kama yenyewe ni shida kuijua takwimu zake. Tunaweza kusema ni ya nne kwa sababu tumbaku imeguswa kwenye kila aina ya saratani kwa sababu ya kemikali zake kuchangia.
“Unaweza kusema asilimia 60 ya saratani inachangiwa na virusi lakini ukija kwenye tumbaku kila saratani imehusishwa na tumbaku,” anafafanua Dk Kahesa. Wakati baadhi ya watu (akiwemo Mshomi) wakijipa moyo kwa kusema ‘mbona watu wengine wanavuta sigara na hawaugui saratani, Dk Kahesa anafafanua kuwa maradhi hayo huchukua muda mrefu hadi kugundulika.
Anasema umri wa sasa wa kuishi kwa Tanzania ni miaka 62 na kipindi kilichopita ilikuwa miaka 52. Hivyo anasema wagonjwa wengi kipindi kilichopita walikuwa ni wazee wenye umri wa takribani miaka 65.
“Kwa hiyo utaona watu wengi walikuwa wanafariki kabla saratani haijatokeza. Kama wangeishi miaka 80 hadi 90 wengi wangegundulika, lakini walikuwa wanatibiwa kwa maradhi mengine kama vile TB (Kifua Kikuu).
Wengine wanasema hawaoni ugonjwa wowote lakini ukweli ni kwamba vifaa vya kugundua saratani ni vya utaalamu wa hali ya juu.” Mbali na saratani, uvutaji tumbaku/ sigara pia unachangia maradhi ya moyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Mohamed Janabi anasema athari kubwa za matumizi ya tumbaku zinakuwa kwenye mishipa ya damu ya moyo. Anafafanua kwamba moyo umezungukwa na mishipa ya damu inayoitwa coronary arteries ambayo sigara huwa inaiharibu.
“Kwa Tanzania bado uvutaji wa sigara siyo tatizo kubwa, bado halijawa kubwa, hatuwezi kuweka sigara katika orodha ya juu. Lakini wagonjwa wetu waulizwe kuhusu sigara kwa sababu ni moja ya magonjwa ya moyo. Asilimia 60 ya mgonjwa anaumwa nini tunaipata katika historia ya mgonjwa.
“Kuna wagonjwa wa moyo hapa ambao unasikia wanavuta pakiti mbili hadi tatu kwa siku, athari yake inakuwa kubwa zaidi, kwanza nafasi yake ya kuharibu mishipa ya moyo inakuwa kubwa sana na uachaji wake unakuwa mgumu kwa sababu mtumiaji atapata kitu kinaitwa withdrawer syndrome ambazo ni nyingi kidogo,” anasema.
Hata hivyo, anasema wagonjwa wanaowahudumia hospitalini hapo kwa sababu ya uvutaji wa sigara ni wachache kulinganisha na wale ambao wanapata tatizo la mishipa ya damu kutokana na mafuta na uzito.
Hata hivyo, Dk Janabi anasema ni muhimu Tanzania kuingilia kati matatizo yatokanayo na tumbaku kabla tatizo halijawa kubwa sana. Anatoa mfano akisema zipo nchi zilizoweka udhibiti wa uvutaji wa sigara.
Mfano Australia, mtu hawezi kuvuta kwenye eneo la chuo, Uingereza huwezi kuvuta kwenye baa na wala kubandika matangazo ya sigara kama vile kwenye mashindano ya magari.
Dk Janabi anasema ndani ya sigara kuna kemikali ya nikotini ambayo ina uraibu (hali ya mwili kuzoea kitu fulani). “Ikikuzoea uachaji wake unakuwa mgumu na ndiyo maana ni muhimu vyombo vya habari vikaendelea kuelimisha watu kuepuka kuvuta sigara kwa sababu ukishaanza kuvuta uwezakano wa kuacha unakuwa mgumu,” anasema Dk Janabi.
Anasema elimu inapaswa itolewe kwa wananchi kuhusu athari za sigara na ndiyo maana kwenye paketi za sigara zimeandikwa ‘uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya yako’. Kwa kuzingatia athari zake, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilitunga Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Tumbaku (WHO FCTC).
Nchi 180, zimeridhia mkataba huo ikiwemo Tanzania iliyouridhia Aprili 2007. Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania kupitia kwa mwenyekiti wake, Lutgard Kagaruki kinasisitiza kuwa tumbaku ni janga la taifa ambalo serikali katika kupambana, inapaswa isaidie wakulima kujikita kwenye mazao mbadala na kuwapatia masoko bora na ya uhakika.
“Kwa kuepuka tumbaku, taifa litakuwa limeokoa kizazi cha sasa na kijacho dhidi ya majanga ya kiafya, kiuchumi, kijamii na kimazingira, yanayosababishwa na kilimo na matumizi ya tumbaku,” anasema Kagaruki.
No comments:
Post a Comment