Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
ameagiza kuwa kampeni ya kupanda na ustawishaji miti isiishie Dodoma
mjini tu bali ienee katika Wilaya zote za mkoa wa huo na hatimaye nchi
nzima.
Makamu wa Rais aliyasema hayo kwenye uzinduzi wa kampeni ya kuufanya mji wa Dodoma kuwa wa kijani.
Makamu
wa Rais alisema upandaji miti si kwa ajili ya kuhifadhi mazingira tu
bali ni fursa ya kiuchumi, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi
ambapo alitolea mfano mti mmoja uliokomaa unaweza kunyonya hadi kiasi
cha kilo 150 za gesi ya hewa ya ukaa kwa mwaka,husaidia kupunguza joto,
kusaidia kuboresha afya zetu za mwili na akili kama tafiti
zinavyoonyesha .
“Ni
dhahiri, kampeni hii ya kuifanya mji wa Dodoma kuwa wa kijani ni kuunga
mkono uamuzi wa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli wa kuhamishia
Makamo Makuu ya Nchi kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma kwa vitendo.”
alisema Makamu wa Rais.
Makamu
wa Rais amewataka Viongozi na Wana Dodoma kuipokea kampeni hii kwa
mikono miwili na kutoa kila aina ya ushirikiano ili kufikia lengo zuri
lililokusudiwa.
Makamu
wa Rais ambaye alihamia rasmi mjini Dodoma siku ya ijumaa tarehe 15
Desemba, 2017 alitoa pongezi kwa Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais
Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba na Ofisi yake kwa kuja na
wazo zuri .
Makamu
wa Rais alisisitiza kuwa hategemei kuona zoezi la upandaji miti lianze
na kuisha leo, na badala yake liwe la kudumu, pia alizitaka manisapaa
zitunge sheria ndogo zitakazoelekeza shule, chuo, taasisi na familia
kuanzisha bustani ndogo za miti zitakayomudu mazingira husika,Makamu wa
Rais aliendelea kusema kuwa ni vyema kupunguza ukataji wa miti kiholela
ambapo alizitaka sheria, kanuni na taratibu zizingatiwe kabla ya kukata
miti na kusema tupande miti kabla ya kukata mti.
Makamu
wa Rais alimalizia kwa kutoa shukrani kwa kampuni ya TATU Mzuka kwa
kujitoa na kuhakikisha kampeni hii inatekelezwa na kutoa wito kwa Bodi
ya Bahati Nasibu ya Taifa ya Tanzania iige mfano na kuelekeza makampuni
mengine ya bahati nasibu yaweze kutoa mchango wake katika shughuli za
kijamii hususan kwenye suala la hifadhi ya mazingira.
Pia
Makamu wa Rais alitoa shukrani kwa Jeshi la Kujenga Taifa Makotopora,
DUWASA, Magereza na Tanzania Forest Services (TFS) kwa kujitoa na
kushiriki kikamilifu kwenye zoezi hili.
Mwisho, Makamu wa Rais aliwataka Wanawake wa mkoa wa Dodoma kuanzisha vikundi mbali mbali vya upandaji.
No comments:
Post a Comment