Takukuru, Waziri Dk Philip Mpango waikaba koo Airtel
SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kuagiza Kampuni ya Simu ya Airtel kurejeshwa serikalini, Waziri wa Mipango na Uchumi, Dk Philip Mpango ameitisha vikao vya mfululizo kutwa nzima jana ili kuanza kuchunguza suala hilo, kwa lengo la kupata majibu.
Katika hatua nyingine, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nayo imesema imeanza kufanya uchunguzi wa kina juu ya suala hilo ili kukamilisha agizo la Rais Magufuli juu ya upatikanaji wa majibu ya sakata la Airtel kwa wakati. Juzi Rais Magufuli alimuagiza Waziri Mpango kuifuatilia Airtel ili kujua ukweli ili umiliki wake urudi serikalini kabla ya kuisha kwa mwaka huu.
Gazeti hili jana lilifanya juhudi za kumpata Waziri Mpango ili kujua mkakati wake wa kulishughulikia suala hilo kutokana na muda mfupi aliopewa na Rais Magufuli na kubaini kuwa kwa siku nzima jana, alikuwa akiendesha vikao vilivyokuwa vinajadili suala hilo. Kupitia simu yake ya mkononi, mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni msaidizi wake aliliambia gazeti hili kuwa Waziri Mpango, alikuwa akihudhuria vikao vinavyojadili suala la Airtel.
“Sijui una shida gani, lakini tangu asubuhi Waziri yupo katika vikao, ni vigumu kwake kuzungumza na wewe wakati huu na nafikiri hata baadaye hataweza, maana vikao hivi haviwezi kuisha mapema. “Kama unavyojua jana kuna maelekezo yaliyotolewa na Rais (Magufuli) kwake, hivyo tangu asubuhi yupo katika vikao vinavyohusu suala hilo, hivyo sina hakika kama unaweza ukapata nafasi ya kuzungumza naye kwa leo,” alisema msaidizi wake huyo.
Takukuru yaanza uchunguzi Katika hatua nyingine, gazeti hili lilimtafuta msemaji wa Takukuru, Musa Misalaba ili kujua ni kwa namna gani taasisi hiyo imeanza kulifanyia kazi suala hilo kutokana na kuonekana wazi kuwepo mazingira ya rushwa, ambapo alisema tayari wameanza kufanya uchunguzi. “Kuhusu suala la Airtel, hata sisi tumesikia agizo la Rais, lakini kama mnavyojua ni suala linalohusu uchunguzi kwa hiyo tumeanza kulishughulikia.
Wakati wowote baadaye tukiwa tayari tutawapa taarifa,” alisema. Bodi ya TTCL yajitosa Aidha, katika hatua nyingine, Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), imeiomba serikali kusaidia kurejeshewa kampuni ya Airtel, kwa kuwa umiliki wake si sahihi na umejaa udanganyifu mwingi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Dk Omar Nundu, alisema hakuna ubishi kuwa Airtel ni mali ya serikali chini ya TTCL, hivyo ni muhimu wakarejeshewa wakati huu, ambao kampuni hiyo imeingia katika mapambano ya kiuchumi.
Alisema itakuwa ni usaliti, iwapo Bodi ya TTCL na uongozi wa kampuni hiyo, hawatautoa hadharani ukweli kuhusu uhalali wa Airtel, na kwamba wamejitoa sadaka kuinyanyua TTCL iweze kupeleka gawio la kutosha serikalini.
Dk Nundu aliyewahi kuwa Waziri wa Uchukuzi katika Serikali ya Awamu ya Nne, alisema dhuluma iliyofanywa kwa kipindi chote cha utendaji wa Airtel itawekwa wazi mbele ya Watanzania na kwamba alichokifanya Rais Magufuli ni kuchokoza na wao wako tayari kutoa ushirikiano ili kampuni hiyo iweze kurudi.
Kwa mujibu wa Nundu, kikao kilichowakutanisha viongozi mbalimbali wakiwemo wa Kampuni ya Celtel na serikali kilichofanyika Agosti 5, mwaka 2005, kilijawa na maamuzi yenye vioja yaliyoifikisha Airtel mahali ilipo sasa.
Alisema kurudishwa kwa Airtel ni vita kubwa, wanayokwenda kupambana nayo kwa sasa huku wakiamini kuwa wapo watakaopata msukosuko, lakini wanachokiamini ni kurejea kwa kampuni hiyo ya Airtel chini ya utendaji wa TTCL.
“Hasara nyingi tumeipata tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo, tumewekeza mitaji mingi, ndio maana tunasisitiza kuwa upo ushahidi kuwa ni mali ya TTCL kwa asilimia 100,” alisema Nundu. Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba alisema uongozi wa TTCL na wafanyakazi wote, wanaiunga mkono Bodi ya TTCL kwa asilimia 100 kutokana na mkakati wake wa kusimama kidete ili kuirejesha Airtel serikalini.
Alisema TTCL imeendelea kujiendesha kwa faida, ambapo alitoa mfano wa robo ya mwaka huu iliyoishia Septemba, ambapo faida iliyopatikana kutokana na mfumo wa uendeshaji ilifikia Sh bilioni 1, huku faida kabla ya kodi ikiwa ni Sh bilioni 2.66, na faida bada ya kodi Sh bilioni 1.8, wakati kodi iliyolipwa ikikaribia Sh milioni 800.
No comments:
Post a Comment